Kwa mama ambaye ana tatizo la kutotoa maziwa ya kutosha wakati wa kunyonyesha, hasa kama tatizo hili halitokani na ugonjwa kama vile kuwa na uvimbe au jipu katika titi, tunashauri kutumia mojawapo ya vyakula vifuatavyo:
1. Tende
Kula tende pekee au tende pamoja na maziwa au juisi ya tende yenye maziwa. Kwa wastani, mama anashauriwa kula robo kilo ya tende kwa siku.
2. Pilipili Manga
Matumizi ya pilipili manga kwa kuiweka kwenye uji au juisi, au kuichemsha yenyewe na kuinywa kama chai, husaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa mama anayenyonyesha.
3. Mbegu za Maboga
Kula mbegu za maboga na boga lake au kutafuna mbegu za maboga zilizokaangwa mara kwa mara kunasaidia uzalishaji wa maziwa kwa wingi.
4. Supu ya Taa/Pweza
Kunywa supu ya samaki aina ya taa au pweza kunasaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa mama anayenyonyesha.
5. Supu ya Ng'ombe, Mbuzi, na Kondoo
Baada ya kujifungua, ni vizuri mama kunywa supu kila asubuhi, hasa supu ya kongoro, nyama ya ng’ombe, au kondoo. Supu hizi ni tiba nzuri kwa mama mwenye matatizo ya kutopata maziwa ya kutosha na pia hurudisha nguvu zilizopotea wakati wa kujifungua.
6. Ndizi za Kuchemsha
Ndizi za kuchemsha ni nzuri sana kwa kutibu tatizo la kukosa maziwa kwa mama anayenyonyesha. Ndizi zinapaswa kuchemshwa vizuri hadi ziwe laini, na hata mtori pia unafaa kwa tatizo hili.
7. Maji
Mama mzazi anapaswa kuwa na tabia ya kunywa maji ya kutosha kila siku kwani nayo husaidia kuongeza maziwa kwa ajili ya mtoto.
8. Uji wa Pilipili Mtama
Inashauriwa mama anywe uji wenye pilipili mtama, kwani zina faida mbili:
- Huondoa makovu yaliyotokana na msuguano wa mtoto tumboni.
- Husaidia kuongeza maziwa ya mama ili kumyonyesha mtoto wake ipasavyo.
9. Mboga za Majani
Mama anapaswa kula mboga za majani kwa wingi kwani zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza maziwa na kuboresha afya ya mama na mtoto.